Jumatano 28 Oktoba 2026 - 20:00
Kujisalimisha kwa Marekani ni Kutoka Katika Mduara wa Imani na Kuukanyaga Uhuru

Hawza/ Ayatullah Araki, akiwahutubia viongozi wa kisiasa wa Iraq, alisisitiza: “Kujisalimisha kwa sera za Marekani ni kutoka katika mduara wa imani na kukanyaga uhuru wa nchi, hakuna shaka kwamba kujisalimisha kwenye sera za Marekani na kuzitii ni mfano wa kuvuka mipaka na kumtegemea dhalimu.”

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Muhsen Araki, mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza na mjumbe wa Uongozi wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, katika ujumbe wake aliowaandikia viongozi wa kisiasa wa Iraq, alisisitiza kwamba; kujisalimisha kwenye sera za Marekani ni kutoka katika mduara wa imani na kukanyaga uhuru wa nchi.

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Kwa viongozi wa kisiasa wa Iraq, Mwenyezi Mungu Mtukufu awaongoze katika njia iliyonyooka:

Iraq yetu pendwa na eneo lote kwa ujumla vinapitia kipindi hatari cha kihistoria, ambacho hakiruhusu kughafilika, kupuuza mambo, kufanya maridhiano yasiyofaa wala uzembe wa aina yoyote. Hii ni kwa sababu kipindi hiki ndicho kinachounda msingi wa mustakabali wa Iraq na eneo lote.

Katika suala hili, kuna kanuni zilizo wazi za kisheria na kiakili ambazo haifai kupuuzwa wala kuvuka mipaka yake. Kanuni hizo ni kama ifuatavyo:

Kanuni ya Kwanza ya Kisheria

Ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Anayesema: 

{وَلَا تَطۡغَوۡا۟ۚ إِنَّهُۥ بِمَا تَعۡمَلُونَ بَصِیرࣱ * وَلَا تَرۡكَنُوۤا۟ إِلَى ٱلَّذِینَ ظَلَمُوا۟ فَتَمَسَّكُمُ ٱلنَّارُ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ ٱللَّهِ مِنۡ أَوۡلِیَاۤءَ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ }

“Wala msivuke mipaka, hakika Yeye anayaona mnayoyatenda, wala msiwaelekee wale waliodhulumu, msije mkaguswa na Moto wa Jahannamu, wala hamna walinzi wengine badala ya Mwenyezi Mungu, kisha hamtanusuriwa.”
(Surat Hud, aya za 112–113).

Hakuna shaka kwamba kujisalimisha kwenye sera za Marekani na kuzitii ni mfano wa kuvuka mipaka na kumtegemea dhalimu, jambo hilo halina matokeo mengine isipokuwa kuangukia katika Moto wa Jahannamu, kupoteza msaada wa Mwenyezi Mungu na kukumbwa na masaibu duniani kabla ya adhabu ya Akhera.

Kanuni ya Pili ya Kisheria: Ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Anayesema:


{وَلَن یَجۡعَلَ ٱللَّهُ لِلۡكَـٰفِرِینَ عَلَى ٱلۡمُؤۡمِنِینَ سَبِیلًا }

“Wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini.”
(Surat An-Nisaa, aya ya 141).

Kujisalimisha huku kwa udhalili, ambako leo tunakushuhudia miongoni mwa baadhi ya wanasiasa wa Iraq, ni miongoni mwa mifano iliyo wazi zaidi ya kuwafungulia njia makafiri kuwatawala Waumini, hii ina maana kwamba kukubali utawala huo bila upinzani ni kutoka katika mduara wa imani, pasipo shaka wala utata.

Kanuni ya Tatu ya Kisharia: Ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu Anayesema:

{یَـٰۤأَیُّهَا ٱلَّذِینَ ءَامَنُوا۟ لَا تَتَّخِذُوا۟ ٱلۡیَهُودَ وَٱلنَّصَـٰرَىٰۤ أَوۡلِیَاۤءَۘ بَعۡضُهُمۡ أَوۡلِیَاۤءُ بَعۡضࣲۚ وَمَن یَتَوَلَّهُم مِّنكُمۡ فَإِنَّهُۥ مِنۡهُمۡۗ إِنَّ ٱللَّهَ لَا یَهۡدِی ٱلۡقَوۡمَ ٱلظَّـٰلِمِینَ}

“Enyi mlioamini! Msiwafanye Mayahudi na Manaswara kuwa marafiki na washirika wenu, wao ni wapenzi na washirika wao kwa wao, na yeyote miongoni mwenu atakayewafanya kuwa marafiki na washirika wake, basi huyo ni miongoni mwao, hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhalimu, basi utawaona wale ambao nyoyoni mwao mna maradhi wakikimbilia kushirikiana nao, wakisema: Tunaogopa tusije tukapatwa na msiba, huenda Mwenyezi Mungu akaleta ushindi au jambo jingine kutoka Kwake, na hapo watakuwa wenye kujuta kwa yale waliyokuwa wakiyaficha ndani ya nafsi zao.”
(Surat Al-Maaidah, aya za 51–52).

Hizi ni kanuni za kisheria zilizo wazi ambazo zinaweka mipaka kati ya chaguo mbili: chaguo la imani na kusimama pamoja na watu wakweli, na chaguo la ukafiri na unafiki, ambalo ni kusimama pamoja na makafiri na madhalimu wenye kiburi.

Leo hii, ninyi mmesimama katika njia panda ya chaguo hizi mbili, na hakuna chaguo la tatu linaloweza kufikiriwa katika suala hili.

Hata hivyo, zipo pia kanuni za kiakili zilizo wazi, ambazo ni misingi inayojulikana na akili. Tutataja baadhi yake:

Kanuni ya Kwanza ya Kiakili

Kuondokana na utawala wa dhalimu mwenye kiburi ni bora kuliko kujisalimisha na kunyenyekea mbele yake, na gharama za kuondokana na utawala huo ni ndogo zaidi kwa kiwango kikubwa.

Uzoefu mwingi unathibitisha ukweli huu. Mfano ulio wazi zaidi ni uzoefu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, ambao mnaushuhudia wenyewe, na uzoefu wa utawala wa Saddam Hussein pia hauko mbali na ninyi.

Kanuni ya Pili ya Kiakili

Kumtii adui hakuleti matokeo mengine isipokuwa kuongeza dhuluma na ujeuri wake.

Ni kosa kubwa sana kwa mtu kufikiri kwamba kulegeza msimamo mbele ya adui kutazuia shari yake, badala yake kama ambavyo mamia ya uzoefu wa kibinadamu wa zamani na wa sasa umethibitisha, hatua hiyo huongeza tu ujasiri wa adui na ukatili wake.

Kanuni ya Tatu ya Kiakili

Maslahi ya kila taifa yanapatikana pale linapokuwa lenyewe ndilo linaloamua sera zake, usimamizi wa nchi yake, uchumi wake, utamaduni wake na mahusiano yake ya kisiasa na mataifa mengine.

Hata hivyo, msimamo tunaoushuhudia kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wa Iraq unafichua kosa kubwa katika uelewa wao wa maslahi ya wananchi wa Iraq, tumesikia kwamba baadhi yao wanadai kuwa maslahi ya Iraq yanapatikana kwa kutii maamuzi ya Marekani!

Je, ni kwa maslahi ya wananchi wa Iraq kutokuwa na mamlaka hata ya kuamua nani awe waziri mkuu, mawaziri na wakurugenzi wao wakuu? Je, ni kwa maslahi ya wananchi wa Iraq mapato yao ya mafuta kumiminika kwenda Marekani huku wao wenyewe wakikosa haki ya kufanya maamuzi kuhusu utajiri na uchumi wao? Je, ni kwa maslahi ya wananchi hawa kunyimwa mamlaka ya kuamua mahusiano yao na nchi jirani, huku wakilazimishwa kukatiza uhusiano nao?

Hii ni pamoja na nchi jirani ambazo zina maslahi makubwa ya pamoja na Iraq, hasa nchi jirani iliyosimama kwa dhati pamoja na Iraq wakati wa mgogoro mkubwa wa nchi hiyo, yaani katika siku ambazo magaidi walioungwa mkono na adui Marekani walipoivamia Iraq. Sasa, baadhi ya wanasiasa wa Iraq wanawezaje kujidanganya na kufikiri kwamba kujisalimisha kwa adui wa Marekani na kuwa adui wa jirani yao aliyekuwa na nia safi zaidi ya kuwasaidia kunaendana na busara na maslahi ya taifa?

Hii ni busara ya aina gani inayoyatoa kafara maslahi ya wananchi wa Iraq katika uhuru wa kisiasa, kiutawala na kiuchumi, huku ikiwatoa kafara marafiki na waungaji mkono wa wananchi wa Iraq ili kuwafurahisha maadui zao? Hawa ni marafiki na waungaji mkono ambao walikuwa tegemeo na msaada wa nchi hii katika siku zake ngumu na za upweke.

Je, si Marekani ndiyo adui mkubwa zaidi wa wananchi wa Iraq, nchi ambayo iliiharibu Iraq na kuwamwaga damu za maelfu ya vijana, wanaume, wanawake na watoto wake?

Je, si Marekani ndiyo iliyoandaa na kuanzisha ISIS, kwa mujibu wa madai yaliyotajwa na rais wake wa sasa? Hili ndilo kundi lililowachinja watoto wa Iraq, kuwafanya watoto kuwa mayatima na wanawake kuwa wakimbizi, kuhalalisha umwagaji wa damu na uporaji wa mali za wananchi wa Iraq, na kutwaa kwa nguvu mamlaka ya nchi hiyo, ardhi yake, anga yake, bahari zake na maeneo yake ya nchi kavu?

Enyi wanasiasa wa Iraq, jueni kwamba wananchi wa Iraq ni taifa lenye heshima na hadhi, ambalo halitakubali kamwe fedheha na udhalilishaji, wala halitaiacha imani na dini yake.

Je, hawa si wale wananchi walioitikia wito wa Marji' wao Mkuu na kusimama kwa wingi wa mamilioni ili kuisaidia dini yao na kuiokoa nchi yao, kiasi cha kumshangaza na kumchanganya adui?

Je, hawa si wananchi wa Hussein na Ali, ambao kwa kumfuata Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein (amani iwe juu yake), waliunda mkusanyiko mkubwa zaidi wa kibinadamu katika historia kupitia maadhimisho ya Arubaini ya Imam Hussein, kwa ajili ya kumuunga mkono aliyedhulumiwa na kusimama dhidi ya dhalimu mwenye kiburi?

Je, hawa si wananchi wa taifa kubwa ambao kwa kipindi cha karne kumi na nne wameshikamana na Wilaya ya Amirul-Muuminina Ali (amani iwe juu yake), na licha ya kujitolea mhanga wengi, mashahidi na hasara za kibinadamu na mali walizopata katika njia hiyo, wameendelea kupambana na dhuluma na ujeuri?

Enyi wanasiasa wa Iraq, tambueni kwamba katika siku za usoni, wananchi wa Iraq watainuka dhidi ya ujeuri wa Marekani na kuuvunja nguvu zake.

Taifa hili litawakataa wale waliokubali udhalilishaji na fedheha ya wananchi wake waliodhulumiwa katika kipindi ambacho Marekani ilikuwa ikitawala hatima na mustakabali wao.

Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na Aliyetukuka, Anasema:

{..وَلَیَنصُرَنَّ ٱللَّهُ مَن یَنصُرُهُۥۤۚ إِنَّ ٱللَّهَ لَقَوِیٌّ عَزِیزٌ}

“Na hakika Mwenyezi Mungu atamnusuru yule anayen nusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.”

(Surat Al-Hajj, aya ya 40).

Naye Amirul-Muuminina Ali (amani iwe juu yake) amesema:

«وَاللَّهِ إِنَّ امْرَأً یُمَکِّنُ عَدُوَّهُ مِنْ نَفْسِهِ یَعْرُقُ لَحْمَهُ‏، وَیَهْشِمُ عَظْمَهُ، وَیَفْرِی‏ جِلْدَهُ لَعَظِیمٌ عَجْزُهُ، ضَعِیفٌ مَا ضُمَّتْ عَلَیْهِ جَوَانِحُ صَدْرِهِ‏. أَنْتَ فَکُنْ ذَاکَ إِنْ شِئْتَ، فَأَمَّا أَنَا فَوَاللَّهِ دُونَ أَنْ أُعْطِیَ ذَلِکَ ضَرْبٌ بِالْمَشْرَفِیَّةِ تَطِیرُ مِنْهُ فَرَاشُ‏ الْهَامِ‏، وَتَطِیحُ‏ السَّوَاعِدُ وَالْأَقْدَامُ»

“Wallahi! Hakika mtu anayempa adui yake uwezo wa kumtawala yeye mwenyewe, mpaka adui huyo akala nyama yake, akavunja mifupa yake na kuirarua ngozi yake, basi huyo ni mtu mwenye udhaifu mkubwa sana, na moyo ulio ndani ya kifua chake ni dhaifu na mwoga mno. Basi wewe, ukiamua kuwa hivyo, unaweza kufanya hivyo, ama mimi, Wallahi, kabla sijampa adui yangu fursa hiyo, nitampiga kwa upanga wa Mashrafia kwa pigo ambalo litafanya vipande vya mifupa ya vichwa kuruka hewani, na mikono pamoja na miguu kukatwa na kuanguka chini.”
(Hotuba ya 34, Nahjul-Balagha).

Wassalaamu Alaykum wa Rahmatullahi.

Mohsen Araki

14 Jumada al-Ula 1448 Hijria
(Sawa na tarehe 3 Aban 1405 katika kalenda ya Hijria ya Jua, inayolingana na tarehe 25 Oktoba 2026).

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha